Vitendo
vya kikatili vimekuwa vikitekelezwa katika sura mbalimbali, ila tukio
la mtumishi wa Mungu, Padri Celestine John Nyaumba, 35, kumgonga kwa
gari makusudi na kumcharanga mapanga mzazi mwenzake ni aibu isiyo na
mfano.
Padri Celestine, anayetoa huduma kwenye Kanisa Katoliki la
Mtakatifu Joseph, Homboro, Dodoma, anatuhumiwa kumtendea unyama huo,
mzazi mwenzake, Selestina Anania Kibena, 35, Jumamosi iliyopita, Kata ya
Kiluvya, Pwani.
Hii ni aibu isiyomithilika kwa sababu padri kufanya
ukatili huo ni kashfa nzito, ongezea kwamba alimfanyia hivyo mzazi
mwenzake, wakati kwa sheria za kanisa, ni mwiko kwa padri kujihusisha na
mapenzi achilia mbali kufikia hatua ya kuzaa.
Aibu hiyo, inapata
uzito zaidi kwa kuwa Selestina (mzazi mwenza wa padri), alikuwa mtawa
(sister), lakini usista ulimshinda baada ya kupata mimba, takriban miaka
minne iliyopita.
TUKIO LILIVYOKUWA
Padri
Celestine, akiwa anaendelea na utoaji wa huduma kwenye Kanisa la
Mtakatifu Joseph, alipata nafasi ya kujiendeleza kimasomo, Chuo Kikuu
cha Ardhi, Kitivo cha Ubunifu na Uchoraji wa Majengo, Dar es Salaam.
Akiwa Dar, Padri Celestine anaishi Mbezi Shamba, wakati Selestina ni mkazi wa Maili Mbili, Dodoma.
Kwa
mujibu wa vyanzo mbalimbali, mapema wiki iliyopita, Padri Celestine,
alimwita Selestina, aungane naye Dar es Salaam, ‘wapumzishane’ kwa siku
chache, kwani inadaiwa kwamba uhusiano wao wa kimapenzi ulikuwa
unaendelea kwa siri.
MPANGO WA KIKATILI
Habari zinatiririsha mambo kama ifuatavyo:
Ijumaa iliyopita, Selestina aliwasili Dar es Salaam na kufikia nyumbani kwa Padri Celestine.
Siku
hiyo (Ijumaa), walizungumza mengi, ikiwemo kupanga mambo mbalimbali
kuhusu maisha yao na mtoto wao ambaye sasa ana umri wa miaka mitatu.
Siku iliyofuata (Jumamosi iliyopita), Padri Celestine, alimwomba Selestina, waongozane kwenda Kiluvya, Pwani.
Selestina hakuwa na shaka juu ya hilo lakini akataka sababu ya kwenda Kiluvya, badala ya sehemu nyingine.
Celestine akamweleza kuwa Kiluvya kuna sehemu nzuri ya kupumzika, vilevile ana jambo la kikazi atalifanya akiwa huko.
UKATILI UKATENDEKA
Ilipofika
usiku wa siku hiyo (Jumamosi), Padri Celestine na Selestina, walianza
safari ya kutokea Mbezi Shamba kwenda Kiluvya, wakiwa na gari aina ya
Suzuki lenye namba za usajili T220 AJN.
“Walipofika Kiluvya, Padri
Celestine ambaye alikuwa anaendesha gari hilo, alikata kushoto kuelekea
porini. Gari likiwa porini kabisa, Padri Celestine alisimamisha kisha
akamwambia Selestina ashuke kuangalia chini, kwani alihisi kuna tatizo,”
kilisema chanzo chetu na kuongeza:
“Selestina alishuka akainama
chini kwenye uvungu wa gari kuangalia tatizo, ile anafanya hivyo tu,
Padri Celestine aliendesha gari kwa spidi ili amgonge Selestina. Bahati
nzuri Selestina aliruka lakini gari lilimgonga kwenye paja la kushoto.
“Baada
ya hapo, Celestine aligeuza gari amgonge tena lakini Selestina
alijirusha sehemu yenye kishimo fulani hivi, kwa hiyo gari lilikuwa
haliwezi kumfikia. Kuona hivyo, Padri Celestine alianza kumpiga mawe
Celestine.
“Pengine aliona yale mawe hayana uzito wa kutimiza kile
ambacho alitaka kukifanya kwa Selestina, kwa hiyo Padri Celestine
alifuata panga kwenye gari, akamfuata Selestina, akamcharanga mapanga
kichwani, kwenye mikono yote miwili na mguu wa kushoto.
“Kabla
hajaendelea zaidi, Selestina alimrukia, purukushani ikaendelea. Padri
Celestine alimng’ata Selestina katika shavu la kushoto, mwanamke huyo
naye akajibu mapigo, akamng’ata padri katika shavu la kulia.
“Baada
ya purukushani ya muda mrefu, Padri Celestine aliona mambo magumu,
ikabidi amwombe msamaha Selestina kwamba shetani alimpitia, akamwomba
ampeleke hospitali.
“Selestina alikubali lakini ile Padri Celestine
anafuata gari, Selestina alijitutumua na kukimbia mbali zaidi, Padri
Celestine aliporudi pale alipomwacha, hakumwona tena.”
HOSPITALI NA POLISI TUMBI
Chanzo
chetu kilisema: “Selestina alijivuta mpaka Hospitali ya Mkoa wa Pwani,
Tumbi. Vilevile alitoa taarifa kwenye Kituo cha Polisi Tumbi.
“Polisi walianza kufanya upelelezi wao na kufanikiwa kumkamata Padri Celestine, Jumapili iliyopita jioni.”
RPC ANENA
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei, alikiri kutokea kwa tukio hilo
na akafafanua kwamba baada ya Padri Celestine kuhojiwa, alisema
alipitiwa na shetani kutokana na usumbufu aliokuwa anaupata kutoka kwa
Selestina.
Kamanda Matei alisema, Padri Celestine alidai kuwa
Selestina alikuwa anamuomba fedha nyingi za matumizi kwa ajili ya mtoto
wao, kwa hiyo shetani alimpanda na kufikia hatua ya kufanya kile
alichokitenda.
SELESTINA NAYE AZUNGUMZA
Akiwa
amelazwa Hospitali ya Tumbi, Selestina alisema: “Nashangaa kwa kila
kilichotokea. Niliitwa na Padri Celestina kuja kupumzika, nashangaa
mapumziko yamegeuka mateso.”
Source: globalpublisher.info
No comments:
Post a Comment